Afrika ya Mashariki ya Kiingereza
From Wikipedia
Afrika ya Mashariki ya Kiingereza lilikuwa jina la eneo la Kenya lililowekwa chini ya utawala wa ulinzi wa Uingereza kuanzia mwaka 1895 hadi 1920 BK.
Wakati wa mashindano ya kugawa Afrika kati ya madola ya Ulaya Kampuni ya Kifalme ya Kiingereza kwa Afrika ya Mashariki ilianza shughuli zake katika eneo hili kwa kibali cha sultani ya Zanzibar kuanzia mwaka 1888. Kampuni hiyo ilitakiwa kuwa na mamlaka juu ya eneo hili kwa kusudi la kufanya biashara lakini uwezo wake haukutosha kutimiza shughuli hasa maandalizi ya kujenga reli ya Uganda kati ya Mombasa na Kampala.
Baada ya kuazimia kujenga reli Uingereza iliona haja ya kulinda eneo la reli hiyo ndipo ikatangaza eneo lote kati ya Mombasa na Uganda kuwa chini ya ulinzi wake kuanzia tarehe 01.07.1895. Huo ndiyo mwanzo wa koloni la Afrika ya Mashariki ya Kiingereza ambalo baadaye liliitwa Kenya. Eneo hilo baadaye lilipanuliwa zaidi hadi kukutana na maeneo yaliyokuwa chini ya utawala wa Italia (Somalia) na Ethiopia upande wa Kaskazini, utawala wa ushirikiano wa Misri na Uingereza (Sudan). Upande wa kusini mpaka ulifuata mapatano na Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.
Mpaka na eneo chini ya utawala wa ulinzi wa Uganda ulisahihishwa mwaka 1905; hadi wakati ule sehemu kubwa ya eneo la Kenya ya Magharibi ya leo ilihesabiwa kuwa upande Uganda.
Baada ya vita kuu ya kwanza hali ya eneo lilibadilishwa kuwa koloni ya Kenya kuanzia 1920.