Bamba la Uhindi
From Wikipedia
Bamba la Uhindi ni bamba la gandunia ndogo katika ganda la dunia. Bara Hindi yenye nchi za Uhindi, Pakistan, Bangla Desh, Nepal pamoja na nchi visiwa Sri Lanka na Maledivi iko juu ya bamba hili.
Bamba la Uhindi limepakana na bamba la Ulaya-Asia, Bamba la Australia, Bamba la Afrika na bamba la Uarabuni.
Lilijisukuma chini ya bamba la Ulaya-Asia takriban miaka milioni 10 iliyopita na kusababisha kujikunja kwa ganda la dunia na kutokea kwa milima ya Himalaya.
Bamba la Uhindi limepimwa kuwa na mwendo wa kuelekea kaskazini wa sentimita 5 kila mwaka. Linaendelea kusukuma dhidi ya bamba la Ulaya-Asia na kuikunja zaidi.
Contents |
[edit] Mitetemeko ya Ardhi
Mwendo huu na msuguano kati ya mababmba husababisha mishtuko inayojitokeza kama tetemeko la ardhi. Kati ya mitetemeko mikubwa ilikuwa:
[edit] Tetemeko chini ya Bahari Hindi ya Krismasi 2004
Tar. 26 Disemba 2004 lilitokea tetemeko kubwa la ardhi chini ya Bahari Hindi kwenye mstari ambako bamba la Uhindi linajisukuma chini ya bamba ndogo la Burma. Siku ile 1,200 km za pembizo la bamba la Uhindi zilisogea mbele katika muda wa dakika chache kwa urefu wa takriban 15 m chini ya bamba la Burma. Bamba la juu lilisukumwa na kupaa juu takriban mita 30. Mshtuko huu ulianzisha wimbi kubwa chini ya bahari lililotokea juu kwa umbo la tsunami lililoua takriban watu 275,000.
[edit] Tetemeko la Kashmir 2005
Tar. 8 Oktoba 2005 mwendo wa bamba la Uhindi chini ya Himalaya ulisababisha tetemeko la ardhi lililoua takriban watu 60,000 na kuharibu nyumba za watu milioni 2.5. Kitovu cha mshtuko kilikuwako karibu na Muzaffarabad katika eneo la Azad Kashmir upande wa Kipakistani ya Kashmir.
[edit] Viungo vya Nje
- The collision of India and Asia (90 mya — present), by Christopher R. Scotese, from the Paleomap Project. Retrieved December 28, 2004.
- Magnitude 9.0 off W coast of northern Sumatra Sunday, December 26, 2004 at 00:58:49 UTC: Preliminary earthquake report, from the U.S. Geological Survey. Retrieved December 28, 2004.
Categories: Jiografia | Gandunia | Asia | Bahari ya Hindi | Jaribio