Walawi (Biblia)
From Wikipedia
Kitabu cha Walawi ni kitabu cha tatu katika Agano la Kale au Biblia ya Kiebrania. (Kitabu cha kwanza ni Mwanzo.) Kwa asili kimeandikwa katika lugha ya Kiebrania, na katika lugha hiyo kinaitwa Wayikra, maana yake “na aliita”, ambalo ni neno la kwanza katika kitabu hicho. Wengine wanakiita Kitabu cha Tatu cha Mose (au Musa) kwa vile inafikiriwa kuwa Mose ni mwandishi wa kitabu hicho. Kwa lugha ya Kiyunani, kinaitwa Levitikon (biblion), maana yake “(Kitabu cha) Walawi (au Makuhani)”.
Kitabu cha Walawi kina sura ishirini na saba, na sura zote zinahusu amri na maagizo ya Mungu kwa Waisraeli. Maagizo hayo yanaeleza sadaka (sura 1-7), walivyowekwa wakfu makuhani wa kwanza, yaani Aroni (au Haruni) na wanawe (sura 8-10), utakaso (sura 11-15), siku kuu ya msamaha wa dhambi (sura 16), na maagizo mbalimbali kuhusu maisha ya kila siku na uendeshaji wa ibada (sura 17-27).