Zaburi (Biblia)
From Wikipedia
Kitabu cha Zaburi ni mojawapo ya vitabu vya Agano la Kale au Biblia ya Kiebrania. Kina sura 150; kila sura ni zaburi moja. Zaburi ni aina ya sala iliyotungwa kama shairi au wimbo.
Kitabu cha Zaburi kinatumiwa na Wayahudi na Wakristo kama kitabu cha sala. Mada za zaburi hasa ni sifa za Mungu, shukrani, huzuni na toba, maombolezo, furaha na imani, elimu ya kidini, na ombi la ushindi dhidi ya maadui wasiomcha Mungu. Zaburi zatufundisha jinsi binadamu awezavyo kuzungumza na Mungu.
Zaburi nyingi zimetungwa kama shairi la Kiebrania; mara nyingi fungu moja linarudia wazo la fungu lililopita, k.m. katika Zaburi 22, mistari 1-2:
- Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?
- Mbona uko mbali sana kunisaidia, mbali na maneno ya kilio changu?
- Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu;
- napiga yowe usiku, lakini nafuu sipati.
Katika kitabu cha Zaburi zaburi fulani zimewekwa pamoja kwa mfano, Zaburi za Wakorahi (baadhi zikiwa 42—49) au za Asafu (73—83), Zaburi za kumsifu Mungu aliye Mfalme au Mtawala wa wote (93—99) au Zaburi za kuhiji (120—134). Baadaye Zaburi ziligawanywa katika vitabu vitano: 1—41; 42—72; 73—89; 90—106; 107—150. Kila kitabu hicho kinamsifu Mungu katika mstari wake wa mwisho: 41:13; 72:19; 89:52; 106:48; na Zaburi yote ya 150. Inawezekana kuwa mgawanyo huo ulifanyika kuiga mgawanyo wa vitabu vitano vya kwanza vya Biblia, yaani vitabu vya Mose.
Baadhi ya Zaburi zinazojulikana sana ni:
- Mateso ya Yesu (22)
- Mungu mchungaji wangu (23)
- Ombi la Msamaha (51)
- Sala kuu ya shukrani (103)
- Kumsifu Muumba (104)
- Mungu ajua yote (139)