Beirut
From Wikipedia
Beirut (pia: Beyrouth; Kiarabu: بيروت) ni mji mkuu wa Lebanon, pia mji mkubwa na bandari kuu ya nchi hiyo. Iko mwambaoni wa Bahari ya Kati. Imekadiriwa kuwa idadi ya wakazi ni kati ya milioni moja na mbili.
Mahali pa mji ni kanda kati ya bahari na milima inayofuatana sambamba na mwendo wa pwani. Kitovu cha kihistoria iko kando la rasi inayoitwa Ras Beirut penye kitovu cha mji wa kisasa kabla ya vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Lebanon kati ya 1975 na 1990.
Kipindi kirefu cha vita hiyo ya ndani kilibadilisha uso wa mji kwatika mengi. Mji ulitenganishwa katika maeneo ya Wakristo na Waislamu hasa. Mitaa mipya ilianzishwa mbali na mstari wa mapigano ujenzi ukaongezeka sana hasa upande wa kaskazini na kuelekea milimani.
Tangu amani ya 1990 mji ulijengwa upya. Lakini mashambulizi ya ndege za Israel wakati wa Julai 2006 yaliharibu tena sehemu za mji.
Kabla ya vita Beirut ilikuwa kitovu cha kiuchumi na kiutamaduni wa Mashariki ya Kati. Nafasi ya kinara cha kiutamaduni imerudishwa kwa sababu ya uhuru kwa ajili ya magazeti na wachapishaji vitabu lakini uongozi wa kiuchumi umehamia nchi za ghuba ya Uajemi kama vile Kuwait, Qatar au Falme za Kiarabu.
Beirut imekuwa tangu muda mrefu kitovu cha elimu katika Mashariki ya Kati. Chuo Kikuu cha Kimarekani (American University of Beirut) pamoja na vyuo vikuu vya serikali na mapadre Wakatoliki vimeendelea kufundisha hata wakati wa vita.
Makala hiyo kuhusu "Beirut" bado ni mbegu. Unaweza kusaidia kuikuza kwa kubofya kitufe kilichoandikwa "hariri". Ikiwepo makala kuhusu Beirut kwa lugha nyingine, unaweza kuitafsiri kwa Kiswahili. |