Bendera ya Afrika Kusini
From Wikipedia
Bendera ya Afrika Kusini ni ya pekee kati ya bendera za dunia ikiwa na rangi sita.
Kimsingi muundo wake ni milia mitatu ya kulala ya nyekundu, kijani na buluu; pamoja na kanda nyembamba nyeupe juu na chini ya mlia wa kijani.
Huu mlia wa katikati (kijani pamoja na kanda neupe) unagawiwa ukionyesha umbo la "Y" ya kulala. Pembetatu ndani ya kichwa cha "Y" ina rangi nyeusi inayotengwa na ijani ya "Y" kwa kanda nyembamba ya dhahabu.
Bendera ilikubaliwa April 1994 baada ya mwisho wa utawala wa ubaguzi wa mbari. Ilitengenezwa na Frederick G. Brownell kama bendera ya muda kwa ajili ya uchaguzi wa April 1994 na kuapishwa kwa Nelson Mandela kama rais wa Afrika Kusini tarehe 10. 05. 1994. Imependwa na watu na kupokelewa katika katiba kama bendera ya kudumu.
Kati ya rangi ni zile za Ethiopia au rangi za Umoja wa Afrika: kijani - njano (=dhahabu) na nyekundu. Bendera inaendeleza pia rangi za bendera ya zamani ya Afrika Kusini iliyotumiwa hadi 1994 yaani machungwa (=dhahabu), nyeupe na buluu.
Vilevile rangi za bendera ya ANC zimepatikana: nyeusi, kijani na njano.
Hakuna maelezo rasmi juu ya maana ya rangi hizi. Lakini mtungaji wa bendera Brownell alieleza mawazo yake wakati wa kutunga hivyo:
- "Y" inaonyesha mwendo wa vikundi, mbari na makabila mengi kuwa taifa moja.
- Nyekundu ni kumbukumbu ya damu iliyomwagika katika historia ya Afrika kusini.
- Bluu ni kwa ajili ya anga (labda mbingu?) inayotazama wananchi wote na bahari mbili zinazozunguka Afrika Kusini
- Kijani ni kumbukumbu ya mashamba na mazingira asilia
- Nyeusi ni ya watu weusi a Afrika Kusini na pia ya kuwa sehemu ya Afrika yote
- Nyeupe ni ya watu weupe wa Afrika Kusini na pia alama ya amani
- Njano / dhahabu hukumbusha juu ya malighafi ya nchi