Agostino wa Hippo
From Wikipedia
Agostino wa Hippo (13 Novemba, 354 – 28 Agosti, 430) alikuwa mwanatheolojia na kiongozi wa kanisa katika Afrika ya Kaskazini wakati wa karne ya 5 BK. Kutokana na maisha, mafundisho na maandiko yake amepewa cheo cha mtakatifu pia cha mwalimu wa kanisa. Hippo ni jina la mji katika Algeria ya leo alipokuwa askofu.
Contents |
[edit] Maisha yake
Agostino alizaliwa mw. 354 BK mjini Thagaste pale Numidia (leo: Algeria) yaani karne mbili baada ya Origine. Jina lake la kuzaliwa lilikuwa Aurelius Augustinus. Wakati ule Ukristo ulikuwa tayari dini iliyokubaliwa katika Dola la Roma. Mateso ya Wakristo yalikwisha. Mama yake Agostino alikuwa Mkristo, Baba mpagani aliyefuata dini ya zamani ya kuabudu miungu mingi. Alipata elimu yake katika Chuo Kikuu cha Karthago (leo: Tunis). Katika sehemu za magharibi za Afrika ya Kaskazini wenyeji wa kiasili walikuwa Waberiberi, lakini watu wa mjini na wenye mashamba makubwa walikuwa wa asili ya Kiulaya wakatumia hasa lugha ya Kilatini. Kwa jumla sehemu hii ya Afrika ilikuwa karibu na utamaduni wa Ulaya ya Magharibi.
Agostino mwenyewe aliendelea kusoma pale Italia baada ya kumaliza masomo yake Karthago. Ndipo hapo akakutana na watu waliomvuta kuwa Mkristo. Akabatizwa akarudi Afrika akabarikiwa kuwa padre akachaguliwa kuwa askofu wa mji wa Hippo pale Numidia mw. 395 B.K.. Aliaga dunia kwake Hippo mw. 430 wakati washenzi Wagermaniki walioitwa Wavandali walipojaribu kuteka mji wake.
Mpaka kifo chake aliendelea kueleza na kutetea imani ya Kikristo kwa maandiko na vitabu vingi. Kwa njia hii amekuwa mwalimu muhimu sana katika Ukristo wa Magharibi (yaani Kanisa la Kiroma-Katoliki na pia katika makanisa ya kiprotestant yaliyotoka katika kanisa hilo.) Kwa mfano Martin Luther alimtaja Agostino kuwa baba yake wa kiroho pamoja na Mt. Paulo.
[edit] Kazi na mafundisho yake Agostino
Kazi kubwa ya Agostino si kuandika maelezo juu ya vitabu na maneno ya Biblia yenyewe alivyofanya Origine. Kazi yake kuu ilikuwa kutafsiri mafundisho ya Biblia katika mazingira ya kiroho, kijamii na kisiasa ya wakati wake. Hapa aliuliza maswali na kutoa majibu yenye umuhimu mpaka leo. Mafundisho yake yamesikika hasa juu ya swali la neema na dhambi halafu juu ya uhusiano wa Kanisa na Serikali.
[edit] Dhambi na neema
Katika mafundisho yake juu ya neema na dhambi ni Agostino aliyetoa mafundisho ya kwamba ubinadamu umo katika dhambi ya asili tangu Adamu. Uhuru wa kibinadamu umepotea katika dhambi ya Adamu, hali hii imerithiwa na watu wote baadaye. Lakini kwa neema yake Mungu hufunua upendo wake kwetu. Alisisitiza ya kwamba si mwanadamu anayemkuta Mungu lakini Mungu ndiye anayemhurumia mwanadamu mwenye dhambi.
[edit] Mji wa Mungu
Juu ya uhusiano kati ya serikali na kanisa aliandika kitabu chake "De civitate Dei" (kwa Kilatini: Mji wa Mungu). Badala ya "mji" tungeweza kutafsiri pia: "eneo au kikundi cha watu au utawala". Alieleza ya kwamba iko "miji" miwili: mji wa Mungu (yaani Yerusalemu wa mbinguni, au kanisa) na mji wa dunia hii, yaani taratibu za kisiasa. Katika "mji wa dunia hii" hali hubadilika. Hakuna taratibu za kudumu. Agostino alifahamu habari za taratibu za Waroma wa kipagani walioangalia makaisari wao kuwa miungu, akafahamu habari za demokrasia ya kigiriki ya kale. Akafahamu habari za mji mkubwa wa Roma ulioitwa "mji wa milele" lakini ulichomwo moto na maadui katika siku zake sawasawa jinsi ilivyoanguka zamani miji ya Babeli au Yerusalemu.
Lakini pamoja na "mji" huo upo "mji" wa pili ndio mji wa Mungu ambao ni mji wa upendo na undugu penye neema yake Mungu.
Miji yote miwili iko pamoja mahali palepale ingawa taratibu zao ni tofauti. Mkristo ndiye raia ya miji yote miwili. Huitwa kuwa mwaminifu katika pande zote mbili. Lakini ajue ya kwamba mji wa dunia hii hauna shabaha ya kudumu. Umeingiliwa na dhambi. Lakini mji wa Mungu utadumu. Umepewa lengo la kudumu, unashirikiana katika enzi ya Mungu.
Hapo ndipo sababu ya kwamba inafaa serikali isikie wazo la kanisa kwani ni kwa njia ya kanisa ya kwamba Mungu ameamua kufunua mapenzi yake. Mkristo anaweza kushiriki katika taratibu za kisiasa akijua ya kwamba mawazo na mipango yote ya siasa havidumu. Utakaodumu ni utaratibu wa Mungu.
Ni kutokana na mafundisho haya ya Agostino ya kwamba Kanisa la Magharibi (yaani Kanisa la Kiroma-katoliki na madhehebu yaliyotokana nalo yaani Waprotestanti) lilijifunza umuhimu wa kuwa na msimamo imara mbele ya serikali mbalimbali zilizojitokeza katika historia ndefu ya kanisa.
Agostino alikuwa kijana aliposhuhudia jinsi gani Mkuu wa Dola Kaisari Theodosio akatubu kanisani. Askofu Ambrosio wa Milan alikuwa amemtenga Kaisari kwani wanajeshi wa serikali waliua watu wengi sana ovyo walipogandamiza fujo lililotokea katika mji wa Thesalonike. Kaisari alimpandisha cheo Mkuu wa jeshi hilo. Watu wengi pamoja na Askofu walisikitika na kuwa na huzuni juu ya tendo hilo. Theodosio alipotaka baadaye kuingia katika ibada Askofu alimtangaza ametengwa kwa sababu ya damu ya wananchi wa Thesalonike hawezi kushiriki meza ya Bwana. Kumbe Kaisari akakubali kosa mbele ya umati akatubu. Hata baadaye viongozi wa kanisa la magharibi wakafuata mara nyingi mfano wa Ambrosio na mafundisho ya Agostino.
Vitabu vyake viwili vingine vya kiteolojia vinavyosomwa hadi leo hasa ni "Maungamo" (kwa Kilatini: Confessiones) na "Kuhusu Utatu" (De Trinitate).
[edit] Urithi wake Agostino
Tunaweza kuona aina mbili za matokeo ya urithi huo:
Kwa upande mmoja kanisa lilijaribu kutawala juu ya jamii na serikali katika nchi za Ulaya. Lilidai sheria zote za serikali zifuate taratibu za kanisa. Viongozi wa serikali walitakiwa kusimikwa na kanisa. Hoja hili huitwa "Uklerikali" (clericalism). Nguvu ya kisiasa ya kanisa lilipingwa na kupinduliwa katika mapinduzi mbalimbali ya Ulaya na Amerika (kuanzia mapinduzi ya Ufaransa 1789, katika mapinduzi ya Marekani ya Kusini karne ya 19 hadi mapigano mengi katika nchi kama Hispania na Austria wakati wa karne ya 20). Siku hizi wazo hili halipo tena lakini zamani lilileta matatizo mengi, kama vile ugandamizaji wa madhehebu mengine na hata vita.
Lakini sehemu nyingine ya urithi huo wa Agostino imebaki: kazi ya kanisa kuzitetea haki za kibinadamu, hata dhidi ya serikali inayoweza kugandamiza haki hizo. Kwa mfano ndiyo makanisa yaliyopinga sana siasa ya ubaguzi wa rangi pale Afrika ya Kusini na zamani pale Marikani, hata dhidi ya serikali iliyotetea utaratibu huo. Vilevile ni makanisa yanayotetea haki za wakimbizi katika nchi nyingi hata kama serikali zimeshachoka na mzigo wa kupokea wageni maskini kutoka nchi zingine.