Karl Peters
From Wikipedia
Karl Peters (27 Septemba, 1856 – 10 Septemba, 1918) alikuwa Mjerumani aliyeanzisha koloni ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.
[edit] Utoto na masomo
Peters alizaliwa mwaka 1856 katika Ujerumani ya Kaskazini kama mtoto wa nane wa mchungaji wa Kilutheri. Baada ya kumaliza shule ya sekondari alisoma historia na falsafa kwenye vyuo vikuu vya Göttingen, Tübingen na Berlin. Akiwa chuoni alivutwa na mafundisho ya Udarwini wa Kijamii yaani mafundisho yanayotangaza ya kwamba ni haki na halali kama wenye nguvu duniani wanatawala na kukandamiza wadhaifu. Baada ya masomo yake ya historia alifanya kazi London (Uingereza) mnamo 1882/1883. Alijifunza mengi kuhusu himaya ya kikoloni ya Uingereza na utawala wake juu ya nchi nyingi.
[edit] Itikadi ya ukoloni
Peters alisikitika kuwa Ujerumani haikuwa na koloni hadi wakati ule. Aliamini ya kwamba koloni huongeza utajiri na enzi ya nchi yenye koloni jinsi ilivyoonekana katika mfano wa utawala wa Kiingereza juu ya India. Alitaka kuwapatia Wajerumani nafasi waliostahili machoni pake kati ya mataifa ya Ulaya.
Aliporudi Ujerumani mwaka 1883 alijishughulisha na siasa ya kudai koloni kwa Ujerumani. Peters alikuwa amejifunza habari za Afrika ya Mashariki alipokaa Uingereza. Hadi wakati ule hapakuwa na koloni za nchi za Ulaya katika Afrika ya Mashariki isipokuwa maeneo ya Wareno katika Msumbiji. Wakati huohuo nchi za Ulaya ziliandaa mkutano wa Berlin Aliamini ya kwamba watu wenye rangi nyeusi ni wadhaifu hivyo wanapaswa kutawaliwa na weupe wenye nguvu
[edit] Peters alianzisha Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Machi 1884 Peters aliunda "Shirika la Koloni za Kijerumani" (Gesellschaft für Deutsche Kolonisation). Wakati ule hapana koloni ya nchji za Ulaya katika Afrika ya Mashariki isipokuwa pwani la Msumbiji lililotawaliwa na Ureno. Himaya ya pekee ya kutambuliwa kimataifa ilikuwa Usultani wa Zanzibar. Kamati kuu ya shirika ilimpa wito wa kupata maeneo katika Afrika ya Mashariki kwa imani ya kuwa utawala wa Zanzibar ni wa pwani tu.
Peters alipoandaa safari yake mataifa ya Ulaya yalikuwa yakiandaa mkutano wa Berlin kuhusu maswala ya Kongo ulioanza Disemba 1884. Mkutano huu ulisababishwa na mipango ya mfalme wa Ubelgiji Leopold II. kujijengea himaya ya binafsi katika beseni ya Kongo akigongana na shabaha za Ureno na Uingereza.
[edit] Safari ya Peters ya Usagara
Tar. 10 Novemba, 1884 Peters alifika Unguja pamoja na wamakamati wawili akaendelea kuzunguka kwenye bara la Tanganyika. Serikali ya Kijerumani ya Chansella Bismarck haikukubali mipango yake kwa sababu iliogopa mvurugo kwenye mkutano ulioalikwa tayari. Peters alipofika kwenye ubalozi wa Ujerumani mjini Zanzibar alipokelewa kwa barua kutoka Berlin iliyosema ya kwamba hawezi kutegemea usaidizi wowote kwani juhudi zake ni nje ya siasa ya
Peters akimwogopa Sultani pamoja na Waingereza alivuka kwa siri kutoka Unguja kwenda bara. Alifaulu kutembelea masultani au machifu kadhaa waliotoa aina ya sahihi kwenye karatasi walizoonyeshwa na Peters. Karatasi hizi ziliandikwa kwa lugha ya Kijerumani zikasema ya kwamba chifu fulani aliweka eneo lake chini ya mamlaka ya shirika la Kijerumani pamoja na kulipatia shirika hili haki ya kutumia maeneo na malighafi yote. Kuna uhakika ya kwamba machifu hawakuelewa walichofanya kwa kuchora alama zao kwenye karatasi hizi; walifikiri ya kwamba walipewa ahadi ya ulinzi kutoka kwa mtawala wa mbali ambaye labda atakuwa na faida kwao siku moja lakini hawakuelewa ya kwamba walitamka kibali kwa wageni kutawala nchi. Peters mwenyewe alisimulia jinsi alivyowapa machifu pombe kali hadi walikuwa tayari kuchora alama zao kwenye karatasi walizoonyeshwa haya bila kuelewa maana yake. Kwa njia hiyo katika muda mfupi kati ya 23.11. - 17.12.1884 Peters alipata hati kutoka machifu ya Usagara, Nguru, Useguha und Ukami kwa ajili ya shirika lake, jumla eneo la 140,000 km².
[edit] Peters kukubaliwa na serikali ya Ujerumani
Peters alirudi Ujerumani Februari 1885 katika siku za mwisho wa Mkutano wa Berlin. Aliomba barua ya ulinzi kutoka serikali kwa ajili ya maeneo aliyodai kuwa chini ya shirika la koloni. Chansella Mjerumani Bismarck aliendelea kumkataa. Hati za Peters aliita karatasi zenye michoro bila thamani ya watu weusi. Lakini Peters alimtisha kuweka maeneo haya chini ya ulinzi wa Leopold wa Ubelgiji aliyekuwa tayari kupanusha himaya yake ya Kongo iliyotambuliwa na serikali za Ulaya wakati wa mkutano. Kutokana na tishio hili Bismarck alikubali na Peters akapewa hati rasmi ya kifalme iliyoweka maeneo ya shirika la koloni chini ya ulinzi wa Dola la Ujerumani.
[edit] Shirika la Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki
Sultani wa Zanzibar hakufurahishwa na habari hizi akapinga kwa telegramu huko Berlin akidai ya kuwa Peters aliingia bila kibali na kufanya mikataba na machifu waliokuwa chini ya Zanzibar. Lakini baada ya kutoa barua za ulinzi Berlin iliona haja ya kusimama imara ikapeleka manowari 8 Zanzibar chini ya admeriKnorr. Sultani alikosa uwezo wa kushindana na jeshi hilo akakubali mikataba ya Peters na kukubali Wajerumani watumie bandari ya Daressalaam.
Wakati huu Peters mwenyewe alibaki Ujerumani na kuandaa upanuzi wa himaya ya shirika lake. Aliunda kampuni mpya ya "Shirika la Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki" iliyochukua nafasa ya shirika la awali. Shirika lilituma maafisa kwa misafara mipya na kuongeza mikataba na machifu hivyo kuongeza eneo lililodaiwa na shirika.
Mwaka 1887 Karl Peters alirudi Afrika kama mkurugenzi wa utawala wa kampuni. Aliingia katika majadiliano na Sultani Barghash ibn Sa'id kuhusu utawala wa pwani. Baada ya kifo cha Bargash mwaka 1888 Peters alifaulu kumshawishi Sultani mpya Khalifa ibn Sa'id kulikodisha eneo lote la pwani kwa Shirika la Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki.
[edit] Msafara wa Emin Pasha na kulenga Uganda
Peters alirudi Ujerumani alipoombwa kuongoza msafara mpya wa kumtafuta Emin Pasha katika eneo kati ya Uganda na Sudan. Emin Pasha alikuwa Mjerumani kwa jina la Dr. Eduard Schnitzer akaingia katika utumishi wa serikali ya Misri, kuwa Mwislamu na gavana wa jimbo la Ikweta katika Sudani ya Kimisri. Baada ya mapinduzi ya Mahdi mwaka 1885 mawasiliano yake Emin Pasha na serikali ya Misri ilikatwa; kamati mbalimbali ziliundwa Ulaya kwa shabaha ya kumwokoa.
Peters alifika tena Afrika ya Mashariki mwaka 1889 akaanza msafara wake Juni 1889 kutoka Witu kwenye pwani la Kenya iliyokuwa eneo lindwa chini ya Ujerumani. Bila Peters na watu wengine kujua Emin Pasha hakuwa na haja lolote la kuokelewa lakini kwa hiari yake alikuwa tayari safarini kuelekea Bagamoyo pamoja na mpelelezi Mwingereza Henry Morton Stanley. Lakini Peters alikuwa na shabaha lake yeye mwenyewe bali na kumtafuta Emin Pasha: kupanusha eneo la shirika lake. Kote alikopita alifanya mikataba mipya na machifu na masultani wa kikabila, kwa mfano tar. 1.2.1890 na chifu wa Kavirondo (Kisumu).
Haya yote alifanya ingawa alijua ya kwamba serikali za Ujerumani na Uingereza ziliwaha kupatana kuhusu maeneo ya Afrika ya Mashariki zilipolenga kutafuta masilahi yao bila kuingiliana. Msafara wa Peters ulipita kabisa katika eneo lililoahidiwa kwa Uingereza. Lakini kufuatana na mapatano ya mkutano wa Berlin wa 1885 utawala wa nchi ya Ulaya katika Afrika ulitambuliwa kama nchi iliweza kuonyesha utawala wake hali halisi. Lakini Waingereza hadi kupita kwa Peters hawakuchukua hatua zozote za kujenga utawala wao katika sehemu za Kenya.
[edit] Mkataba na Buganda
Kilele cha juhudi za Peters kilikuwa mapatano na Kabaka Mwanga II wa Buganda ya Machi 1890. Mwanga hakupendezwa na wamisionari Waingereza na Wafaransa walioshindana kati yao juu ya athari kubwa katika Buganda. Labda kwa matumaini ya kwamba huyu mfalme wa Ujerumani asiyejulikana kwake angekuwa msaada dhidi ya siasa za Waingereza lakini atakuwa mbali mno ili asilete hasara Kabaka alitia sahihi kwenye mapatano ya urafiki na ulinzi kati ya Ujerumani na Buganda. Tendo hili lilitekelezwa na Karl Peters bila kibali wala ujuzi wa serikali yake nyumbani.
Peters alirudi kutoka Buganda kuelekea pwani. Tar. 20. 6. 1890 alikutana na Emin Pascha huko Mpwapwa aliyekuwa tayari njiani kurudi kwake Ikweta. Mwezi wa Julai 1890 Peters alifika Bagamoyo.
[edit] Jinsi alivyotendea Waafrika
Katika msafara huu tabia za Peters zilijionyesha jinsi alivyodharau Waafrika. Aliamini na kuandika mwenyewe ya kwamba Mwafrika hutawaliwa kwa kiboko tu. Kwake Mwafrika hakuwa mtu kamili. Akiona yeye mwenyewe ni Bwana na wenyeji wanapaswa kumtumia aliwadharau. Alipopita Ugogoni alikasirika juu ya Mgogo aliyecheka alipomtazama wakati Peters alipojinyoa ndevu. Peters aliamuru apigwe kiboko. Tendo hili liliwasababisha Wagogo kuchukua silaha ikawa vita watu wakauawa kwa wengi. Watu waliosafiri naye na kumjua Peters walisimulia jinsi alivyowapiga mara nyingi mahamali au watumishi wake akapewa nao jina “mkono damu”.
[edit] Mwisho wa himaya ya Peters na shirika la koloni
[edit] Uasi kwenye pwani dhidi ya utawala wa shirika
Wiki chache tu baada ya Peters kuanzisha safari yake ya kumtafuta Emin Pasha utawala wa shirika lake liliporomoka vibaya. Shirika la Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki ilianza kutekeleza mapatano na Sultani wa Zanzibar kuhusu utawala wa pwani kuanzia Agosti 1889. Kushushwa kwa bendera ya Sultani na kupandishwa kwa bendera ya shirika kulishtusha wenyeji wengi. Maafisa Wajerumani wa shirika walionyesha ukali wakidai utawala juu ya mabandari. Haya yote yalisababisha mara moja ghasia. Wenyeji wakaongozwa na watu kama Abushiri na Bwana Heri. Uasi ulianza Pangani na kuenea kote pwani na kuwa vita kabisa. Shirika lilishindwa kupambana na upinzani huo wa wenyeji.
Hapo seriali ya chansella Bismarck iliingilia kati na kutuma manowari pamoja na wanajeshi waliokandamiza upinzani wote. Maeneo ya shirika yaliwekwa chini ya serikali ya Ujerumani kama koloni ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Utawala wa shirika la Peters ulikwisha.
[edit] Mkataba wa Helgoland-Zanzibar kuingilia kati
Karl Peters aliporudi pwani mwezi wa Julai 1890 alipokea habari hizi pamoja na habari za mkataba wa tarehe 01.07.1890 kati ya serikali za Uingereza na Ujerumani zilimoelewana juu ya mipaka ya maeneo yao katika Afrika. Waingereza walikuwa wakishtushwa na matendo ya Peters ya kulenga Uganda. Serikali mpya ya Ujerumani ya chansella Caprivi iliona kuwa uhusiano mzuri na Uingereza ni muhimu kushinda kuongeza koloni zilizotazamiwa na mashaka na sehemu ya wanasiasa Ujerumani.
Katika mkataba huu ulioitwa wa „Helgoland-Zanzibar“ Wajerumani walikubali kuwa Uganda, Zanzibar na nchi kaskazini ya mstari kati ya Ziwa Viktoria Nyanza na mlima Kilimanjaro pamoja na Witu yawe maeneo chini ya athira ya Uingereza. Waingereza waliahidi ya kwamba watamshawishi Sultani wa Zanzibar kuwapatia Wajerumani pwani la sehemu iliyoitwa baadaye „Tanganyika“. Mapatano mengine yalihusu mipaka kati ya maeneo ya Waingereza na Wajerumani huko Afrika ya Magharibi na kisiwa cha Helgoland katika Bahari ya Kaskazini.
Peters aliona ya kwamba safari yake ilikuwa bure kabisa. Alisikitika na kufoka dhidi ya wanasiasa huko Berlin. Aliporudi Ujerumani tena alijiunga na wengine waliodai siasa kali ya ukoloni akawa mmojawapo wa waanzilishaji wa „Jumuiya ya Wajerumani Wote“ (Alldeutscher Verband). Jumuiya hii ilitangaza utaifa mkali, chuki dhidi ya mataifa majirani, vilevile dhidi ya Wayahudi, dhaurau dhidi ya watu wenye rangi tofauti na madai ya kuwa Ujerumani ilistahili maeneo makubwa zaidi katika Ulaya na katika mabara mengine.
[edit] Unyama wa Peters Kilimanjaro na kufukuzwa kwake
[edit] Kamishna wa Kaisari
Baada ya kurudi kwake Peters Berlin sehemu ya wanasiasa na magazeti walimshangilia na kumsheherekea kama shujaa wa kitaifa aliyezuiliwa na waoga serikalini waliothamini uhusiano na watu wa nje kama Waingereza kuliko masilahi ya taifa.
1891 serikali iliamua kutumia maarifa ya Peters ilimpa cheo cha „Kamishma wa Kaisari katika eneo la Kilimanjaro“. Kazi yake kuu ilikuwa kuelewana na Waingereza kuhusu mwendo kamili ya mpaka kati ya sehemu za Wajerumani na Waingereza. Menginevyo alikuwa mkuu wa utawala wa kikoloni wa eneo hili.
[edit] Mapenzi na mauti
Akiwa mwakilishi Mjerumani Kilimajaro Peters alikuwa na mabinti wenyeji aliyowatumia kama wapenzi wake. Usiku wa tar. 18.10.1891 Peters alimkuta binti Yagodja pamoja na Mabruk mtumishi wa kiume wakilala pamoja. Peters alikasirika mno akaita tar. mara moja kamati ya mahakama akiwa yeye mweyewe mwenyekiti. Mtumishi wake Mabruk alihukumiwa anyongwe. Yagodja alikimbia lakini alikamatwa katika mwezi wa kwanza 1891. Alipigwa viboko na kunyongwa naye.
Katika hasira yake Peters aliamuru hata kijiji cha binti katika eneo la Rombo kichomwe moto. Wachagga wa Rombo walichukua silaha na kujitetea. Hasira ya Peters ilisababisha vita ya miezi kadhaa, vijiji vingi viliharibika na watu kufa.
[edit] Kesi dhidi ya Peters
Aprili 1892 gavana Mjerumani von Soden mjini Daressalaam alipokea barua kutoka kwa mmisionari Mwingereza Smythies alimoandika sababu za vita Kilimanjaro kuwa ni unyama wa Peters. Von Soden alifanya utafiti akatuma taarifa juu ya matendo ya Peters kwenda Berlin. Gavana aliandika ya kwamba katika maoni yake hukumu za mauti hazikuwa na haki kwa sababu Peters alitumia madaraka yake vibaya kwa kiburi na kisasi cha binafsi.
Awali serikali ya Berlin ilipendelea kutochukua hatua dhidi ya Peters. Gavana von Soden aliona aibu ya kuwa Peters alitenda maovu haya wakati yeye ana wajibu kwa ajili ya koloni lakini hakuwa na uwezo wa kumwondoa madarakani kwa sababu ya cheo chake Peters. Von Soden alisisitiza mwishoni akajiuzulu na kuacha cheo chake mwaka 1893.
Mambo yalibadilika baada ya wabunge wa upinzani katika „Reichstag“ kupata habari zake Peters na kupeleka maswali bungeni. Peters aliitwa arudi Berlin akapewa kazi wizarani. Kamati ya nidhamu ilifungua kesi dhidi ya Peters na kumfanyia utafiti.
Peters alipoona mambo yanaweza kwenda vibaya aliomba kupumzika akahamia London. Kamati ya nidhamu iliamua tarehe 24.04.1897 kuwa Peters alikosa. Alifutwa katika utumishi wa serikali pamoja na kupoteza haki za pensheni (malipo ya uzeeni). Mahakama kuu ya nidhamu ilirudia tamko hili vikali zaidi Peters alipotafuta rufaa.
[edit] Maisha ya Peters baada ya kuondolewa katika utumishi wa serikali
Alipokaa tena London Peters aliunda makampuni ya kutafuta dhahabu katika Afrka ya Kusini. Alisafiri mara sita kwenda Zimbabwe, Msumbiji na Afrika Kusini. (Dr. Carl Peters Estates and Exploration Co. na South East Africa Ltd.).
Mwaka 1905 Kaisari Wilhelm II aliyekuwa mshabiki wa Peters alimpa haki ya kutumia tena kwa heshima yake cheo cha “Kamishna wa Kaisari”.
Mwanzo wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia alirudi Ujerumani kwa sababu kampuni zake katika himaya ya Uingereza zilinyimwa kama mali ya kiadui. Kaisari alimsaidia tena kwa kumpa pensheni kutoka makisio yake ya binafsi.
Karl Peters aliaga dunia kabla ya mwisho wa vita tar. 10 Septemba, 1918. Hakukumbukwa sana isipokuwa na vikundi kadhaa vilivyodai Ujerumani irudishwe koloni zake zilizonynang’anywa baada ya vita.
Tangu 1933 serikali ya Adolf Hitler ilimkumbuka na kumheshimu ikimtambua kama mtangulizi wa itikadi yake. Barabara na viwanja katika miji mbalimbali vimepewa jina lake. 1963 Adolf Hitler aliatamka kwa amri ya pekee kuwa hukumu dhidi ya Peters ifutwe na mjane wake apewe pensheni yake.
Katika miaka ya nyuma barabara zilizoitwa kwa mujibu wa Peters zilibadilishwa jina wa sababu miji kadhaa iliona ya kwamba ni aibu kutunza kumbukumbu yake kwa njia hii.
Nchi za Afrika | |
---|---|
Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad |Cote d'Ivoire | Djibouti | Eritrea | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesoto | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Uhabeshi | Uswazi | Zambia | Zimbabwe | |
Maeneo ya kiafrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika | |
Ufaransa: Mayotte · Réunion | Hispania: Visiwa vya Kanari · Ceuta · Melilla | Ureno: Visiwa vya Madeira | Uingereza: · Kisiwa cha St. Helena · Kisiwa cha Diego Garcia |